Thursday 22 June 2023

Waziri Mkuu Ajitosa Sakata La Mwanafunzi Kupotea.

Waziri Mkuu ajitosa sakata mwanafunzi kupotea, ataka uchunguzi
June 22, 2023Admin
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameingilia kati sakata la mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Panda Hill, Esther Noah aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha akimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kufanya uchunguzi zaidi kwa haraka.

Ester anadaiwa kupotea Mei 18, mwaka huu, akiwa katika mazingira ya shule hadi sasa zimepita siku zaidi ya 20 bado hajaonekana licha ya jitihada za kutafutwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mbeya.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu leo Alhamisi Juni 22, 2023, imeeleza kuwa Majaliwa amefikia uamuzi huo baada ya kupokea ‘clip’ fupi yenye sauti ya mzazi wa binti huyo aliyekuwa akisoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne kisha kidato cha tano mchepuo wa sayansi (PCB).

Katika clip hiyo, mzazi huyo anadai kuwa yeye na mumewe waliitwa na uongozi wa shule hiyo na kujulishwa Esther hajaonekana tangu asubuhi ya Mei 18, 2023 na kwamba hadi sasa zimepita siku zaidi ya 20 wamekuwa wakimtafuta binti yao kila mahali lakini hakuna dalili za kumpata.

Amesema baada ya kufika shuleni hapo walielezwa kuwa chanzo cha mtoto wao kutoroka ni baada ya kubainika kuwa na kitabu cha kuangalizia majibu mtihani uliokuwa ukifanyika ambao ni wa muhula. Baada ya kubainika Esther alinyanga’nywa na kuchaniwa mtihani wake na kupewa karatasi nyingine.

“Esther alifanya tena mtihani, lakini shule wana utaratibu wa adhabu za viboko ambapo alichapwa vitatu na kuendelea na mitihani mingine. Lakini ilipofika jioni inadaiwa Esther alionekana kanisani akiwa analia, lakini marafiki zake waliomuona walidhani analia kwa sababu ya maombi.

“Lakini wanafunzi wengine mashuhuda walisema walimuona mwanangu akiwa na note book, kanisani akiandika. Kwa maelezo ya mwalimu siku hiyo asubuhi baada ya kuingia darasani wanafunzi wawili hawakuonekana, akiwamo Esther ambapo Mtawa aliamua kwenda kumuangalia katika bweni lakini hakumkuta,” anasimulia mzazi huyo.

Amesema baada ya taarifa hiyo walitoa taarifa Polisi kuhusu kupotea kwa mtoto wao akiwa shuleni, wakiomba taratibu mbalimbali ziendelea ikiwemo viongozi wa Panda Hill kuhojiwa hasa kitendo cha Esther kutoroka kwa sababu ya adhabu.

Mzazi huyo anadai Mei 17 asubuhi kuna ujumbe wa maandishi uliaandikwa kukutwa madhabahuni ukiwekwa katikati ya daftari. Ujumbe huo unadaiwa kuandikwa na Esther akiwaaga rafiki zake na kuomba Mwalimu Jimmy aache kuwafanyia wanafunzi wengine kitendo alichomfayia yeye kwani kimesababisha maisha yake kuwa magumu.

“Naomba umfikishie salamu Mwalimu Jimmy, mwambie ameyafanya maisha yangu kuwa magumu sana hapa shuleni. Asiendelee kuwafanyia wanafunzi wengine kama alivyoyafanya maisha yangu mimi kuwa magumu,” amesema mama yake Esther akisoma sehemu ya ujumbe huo.

Ameongeza kuwa “Huu ujumbe aliandika kwa lugha ya kishwahili na kiingereza akiwaaga rafiki zake na kuwaambia kwamba anakwenda kuwa peke yake. Tukio hili ni kubwa hatujui mtoto wetu yuko wapi tumezunguka Mbeya yote bila mafanikio hadi mochwari,” amesema.

Mzazi huyo amesema licha Polisi kumhojiwa Mwalimu Jimmy lakini bado hawajafanikiwa kumpata Esther na wamezunguka katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenda kwa ofisa upelelezi wa wilaya na mkoa hadi mkuu wa mkoa (Homera), aliyewarudisha kwa mkuu wa wilaya.

Amesema katika kumtafuta Esther walifika hadi soko la Tunduma ambapo wanafunzi wanakaa na kufanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato, lakini hawakufanikiwa kuumuona binti yao.

“Tumetembea na picha yake hadi katika vijiwe lakini hatujafanikiwa kumuona Esther, hatujui yuko maana aliondoka na sare za shule. Tuna kilio kikubwa maana hatujui yupo hai au amekufa,”anasimulia mzazi huyo kwa sauti ya upole.

0 Comments:

Post a Comment